NIDHAMU YA FEDHA(UKIHESHIMU FEDHA ITADUMU NA KUONGEZEKA
Fedha ukiiheshimu ni rahisi nayo ikakuheshimu kwa kutekeleza mambo mazuri unayoyahitaji, ila kama hautakuwa na nidhamu nayo ni dhahiri kuwa haitaweza kukaa kwako. Fedha huwapenda, huwaheshimu na kuishi na watu ambao wananidhamu nayo.
Watu wengi wanashindwa kufanikiwa kwa kutokuwa na nidhamu ya fedha katika kuishi kwao, na kwao fedha huchukulia kama ni kitu cha kawaida kawaida. Ukweli ni kuwa watu wote waliofanikiwa katika ulimwengu huu ni watu ambao wamekuwa wakiishi kwa nidhamu ya fedha.
“Fedha ni kama maji ya mfereji, ukiyawekea mkondo ni lazima yajae, na upita na kujaa kulingana na ukumbwa na upana wa mfereji, kama haujaweka mfereji haziwezi kuja kwako.”
Kwenye maisha usije kujitia moyo kuwa nikipata kiasi Fulani cha fedha ndipo utafanikiwa na ndoto zako zitatimia, huku ni sawa na kuwa na mipango hewa ambayo si rahisi kuja kutimia kwenye maisha yako, usisubiri mpaka upate milioni 10 ndipo uanze kufanya mambo makubwa, anza na hiyo ndogo unayoipata na katika hiyo unaweza ukafanya mambo makubwa.
Nidhamu ya fedha inajumuisha uwekaji akiba, watu wengi wamekuwa na tamaduni ya kutumia fedha bila kuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba ili ije kuwasaidia kwa ajili ya mambo ya msingi kwa baadae. Mambo ya msingi kuyafahamu kuhusu kujiwekea akiba:-
- Weka fedha kabla hujaanza matumizi yoyote. Kila upatapo fedha anza kuigawa katika mafungu stahiki kabla hujaanza matumizi yake, yaani fungu la kumi, sadaka ya wiki au mwezi, matumizi ya nyumbani kwako na kisha weka kiasi kingine kama akiba. Usianze matumizi kabla haujaweka akiba na kufanya mgawanyo mwingine wa msingi. Katika eneo hili zingatia kuwa uhifadhi bora ni ule unaofanyika kabla ya matumizi na si baada ya matumizi.
- Uwe na malengo juu ya fedha unayoiweka. Ukiweka fedha bila kuwa na malengo yoyote nayo ila unaweka tu kwa kuwa umefundishwa au umeambiwa, kuna uwezekano mkubwa sana ukazitoa siku yoyote na ukazifanyia kitu chochote na bado ukaona ni sawa tu kwa kuwa hazikuwa na malengo. Fedha isiyo na malengo ikifanya kitu chochote bado itakuwa imefanya kitu sahihi. Malengo utakayokuwa umejiwekea juu ya hiyo fedha ndiyo chachu ya kuongeza speed yako katika kuhifadhi.
- Weka fedha yako mahali salama.Wengi hawajiwekei akiba kwa kusingizia kuwa kiasi cha fedha wanazomiliki ni ndogo sana kuzipeleka benki ila kuna mifumo mingi ya kujihifadhia fedha na siku hizi kuna kuweka kwenye mitandao ya simu na hata vibubu (visanduku). Kuhifadhi fedha ni nidhamu ukiwa nayo waweza weka popote na usiitumie mpaka malengo yatakapokuwa yamefikiwa.
Mwandishi Christopher Westra katika kitabu chake cha “I create miliions” anapendekeza njia mojawapo ya kukusanya fedha za kufikia malengo yako ni njia ya kuweka fedha zako katika bahasha mbalimbali zenye mlengo wa kufikia lengo hilo. Kwa mfano ukawa na malengo ya kununua kiwanja, kununua gari, na kununua makochi ya ndani, ili kutimiza lengo unaweza kuchukua bahasha zako 3 na juu ya kila baasha ukaandika fedha hiyo inapaswa kununua nini, yaani zikawa na maneno kama kiwanja, gari, na makochi, baada ya kuwa na bahasha hizo unatengeneza utaratibu wa kuweka fedha ndani ya bahasha hizo taratibu, kwa mfumo wa siku, wiki au mwezi. Uhifadhi wa fedha kwa namna hii utakuongezea ujasiri kuwa lengo lako litakuja kutimia tu.
Mbali na nidhamu ya fedha katika eneo la kujiwekea akiba, eneo jingine la muhimu sana ni eneo la matumizi. Mambo ya msingi kuyazingatia kuhusu matumizi:-
- Usitumie zaidi ya kipato chako.
- Usianze matumizi kabla hujaweka fedha ya akiba, hujatoa fungu la kumi na sadaka (utoaji ni siri ya kuongezewa)
- Achana na manunuzi ya vitu ambavyo si vya msingi kwako. Kuna aina ya vitu ambavyo wengi hupenda kuvimiliki kwa lengo la kujitwalia utukufu kwa wengine.
- Usitumie fedha kwa kuiga wengine wanavyotumia. Hata kama watakusema na kukuita bairi wewe usijali kwa kuwa kuna siku watakuelewa.
- Usinunue vitu ambavyo hukupanga kununua. Epuka mara kwa mara kununua vitu kwa sababu tu umekiona na ukakipenda nani kwa ghafla wala hukupanga hawali, hii ni kwa sababu fedha hiyo utakayoitoa itaacha pengo na ili kuliondoa hilo pengo utapaswa kukopa.
- Jinyime leo kwa manufaa ya kesho. Mafanikio yanahitaji kulipiwa gharama na kuna msemo unasema “no gains without pains” ukiwa na maana ya kuwa hakuna mafanikio pasipo maumivu. Kama kweli unataka kufanikiwa kwenye maisha yako ni lazima ujifunze kulipa gharama ya kuyafikia hayo mafanikio. Ukiacha kutumia pesa yako kwenye hiko kitu kinachokula fedha nyingi leo ukijipa muda utajikuta umefanya mambo makubwa. Wengi walioweza kujinyima na kuwa na nidhamu katika matumizi yao mafanikioimekuwa sehemu ya maisha yao.
Ukiweza kuishi kanuni hizi si rahisi ukawa mtu wa madeni na inawezekana ukawa mkopeshaji na si mkopaji.
Tags
UJASIRIAMALI